Kufuatia suala la utalii wa ndani kuendelea kuzorota katika nchi nyingi za Afrika,baadhi ya asasi binafsi na makampuni ya utalii Tanzania,yameanza kutafuta mikakati ambayo itasaidia kuamsha ari ya raia kutembelea vivutio vyao na kuachana na dhana kudhani kuwa utalii ni kwaajili ya wanaotoka nchi za Ulaya tu.
Nchini Tanzania kampuni ya Utalii ya Kili Base Adventures imezindua Tamasha maalumu linalotarajiwa kufanyika kila mwaka ambapo katika tamasha hili mwana ndondi mstaafu wa ngumi za kulipwa Rashid Matumula anatarajiwa kuongoza hamasa hiyo ambayo itahitimishwa na watalii wazawa kuupanda mlima Kilimanjaro.
Sifael Malle ni mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya Kili Base Adventures,ambaye ameiambia BBC kuwa kutokana na utafiti wao wamebaini kuwa raia wengi katika nchi za Afrika Mashariki hawaoni umhimu wa kufanya utalii wa ndani japo kuwa hawana ueledi mkubwa wa vivutio vilivyo katika maeneo yao.
“Unajua mfano kama Tanzania mtu unakuta kuzaliwa hadi kufikia uzee wake hajawahi fika kwenye vivutio,lakini mbaya zaidi ni pale wanapokuwa nje ya nchi zao unakuta mtu anaulizwa kivutio kilicho katika nchi yake haelewi wakati watu wanatoka katika mabara ya mbali wanafahamu mfano mlima Kilimanjaro ama hifadhi ya taifa”amesema Malle.
Akizungumzia serikali za Afrika na Afrika Mashariki katika mikakati ya kuhamasisha utalii wa ndani,mkurugenzi huyo wa kampuni ya Kili Base Adventure anasema zinapaswa kuwana mikakati zaidi ili kuweza kuamsha ari ya wananchi wake kuona umhimu wa kufanya utalii wa ndani.
Tamasha kama hili ambalo safari hii itaongozwa na mwana masumbwi Rashidi Matumla linatarajiwa kufanyika kila mwaka siku za kuelekea sikukuu ya Pasaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni