Mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa ameshtakiwa kwa utovu wa nidhamu baada yake kulishwa kadi nyekundu Jumamosi wakati wa mechi dhidi ya Everton.
Mhispania huyo alifukuzwa uwanjani baada yake kumkaripia kiungo wa kati wa Everton Gareth Barry dakika ya 84 kwenye mchezo huo ambao Chelsea walilazwa 2-0 uwanjani Goodison Park.
Costa, 27, alionekana kumuuma Barry wakati wa kisa hicho, ingawa wachezaji wote wawili wamekanusha kwamba hilo lilitokea.
Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) hata hivyo limemfungulia mashtaka Costa kutokana na vitendo vyake baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.
"Inadaiwa kwamba vitendo vyake, baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano, ni utovu wa nidhamu,” FA imesema kupitia taarifa.
Mchezaji huyo ana hadi saa 18:00 GMT Alhamisi, tarehe 17 Machi kujibu madai hayo.
Aidha, amepewa hadi Jumatano kutoa ufafanuzi kwa FA kuhusu ishara aliyoitoa kwa mashabiki wa Everton alipokuwa akiondoka uwanjani wakati wa mapumziko.
Source: BBCSwahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni