Mzozo mpya umeibuka kati ya wadau wa klabu ya Simba nchini Tanzania siku chache tu baada ya kampuni ya kamari ya Sportpesa, kutangaza udhamini wake wa klabu hiyo.
Sportpesa, ambayo tayari inazidhamini timu za ligi kuu ya soka nchini Kenya, Gor Mahia na Afc Leopards, imetia mkataba wa miaka mitano na ''wekundu wa msimbazi'' wiki iliyopita kama njia ya kuboresha timu hiyo.
Lakini, Taratibu za Mkataba huo zinaonekana kutomridhisha mmoja wa wekezaji wa timu hiyo, Mfanyibiashara Mohammed Dewji, Maarufu MO Dewji.
MO amefichua kughadhabishwa kwake na hatua hiyo ya kusaini mkataba iliyotekelezwa bila kuhusishwa kwake.
''Inasikitisha kwa uongozi wa Simba kusaini mkataba wa muda mrefu bila kusaka ushauri wangu''. Aliandika kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter.
Hata hivyo, klabu ya Simba, haijajibu madai hayo kufikia sasa huku ikieleza kuwa inamakinika kwenye mechi zake zijazo za ligi kuu ya Tanzania bara kabla ya kutoa kauli rasmi.
Kwenye ukurasa wake rasmi wa Instagram, Simba imeahidi kufafanua zidi juu ya kinachoendelea kwenye timu hiyo. Kupitia taarifa ya makamu wa rais, Geofrey Nyange, Simba iliandika,
''Uongozi utatoa tamko katika muda muafaka juu ya suala hili la muingiliano wa mkataba wa Sportpesa na uwepo wa MO ndani ya Simba SC. Tuna mechi mbili mbele yetu ambazo ni muhimu zaidi kwa sasa. Tunaomba utulivu na uvumilivu wenu. Natanguliza Shukrani''.
Wakati huo huo, msemaji wa timu hiyo, Haji Manara, ambaye alishiriki kwenye hafla ya kuzindua mkataba huo mjini Dar Es Salaam, ameonekana kujiondolea lawama kutokana na hisia zinazoendelea kutolewa kuhusu mpango huo.
Kupitia ukurasa wake wa instagram, Haji amejitetea kuwa 'anapokea lawama zisizomhusu na kuwa ana nguvu za kuhimili lawama zote.
''Uongozi wowote ni Jalala ila uongozi wa mpira ni DAMPO, mara nyengine napokea lawama hata zisizonihusu, lakini nina moyo wa chuma na uzoefu wa kuwa kiongozi katika tasnia tofauti, kazi yangu ni kuhabarisha umma,mengine ni kunionea'',. Alichapisha.
Kwa sasa, Simba inashikilia nafasi ya pili kwenye ligi baada ya mechi 29 ikiwa na alama sawa na viongozi Yanga wanaowazidi kwa magoli
Source:BBCSwahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni