Mwanamke mmoja ambaye anaugua saratani ya matiti amejioa mwenyewe baada ya kusubiri mchumba kwa muda mrefu.
May
Chen mwenye umri wa miaka 28 kutoka Taiwan ameambia BBC kwamba anaugua
ugonjwa huo lakini hajakubali sababu hiyo kuhujumu ndoto yake ya
kuolewa.''Nimekuwa nikisubiri mtu kujitokeza na kusema kwamba angependa kufunga ndoa nami mbali na kupiga picha za harusi nami aliambia BBC .
Anasema kwamba wakati unapohisi kwamba huna miaka mingi ya kuishi huna budi kujifanyia maswala ambayo yamekuwa ndoto yako.
Anasema kwamba ameamua kuafikia ndoto yake kupitia kupiga picha za harusi. Alijichagulia marinda yote manne na vito alivyovaa.
Anasema kuwa wapiga picha walimshauri kupiga picha katika studio lakini yeye akawaambia kwamba anataka picha sawa na zile za harusi.
Hivyobasi alikodisha gari na kwenda kupiga picha hizo katika maandhari ya harusi.
''Nilipovalia rinda la harusi nilijawa na hisia mpaka nikahisi kulia''.
Anasema kwamba alihisi kana kwamba ameafikia ndoto yake ya miaka mingi.
Kwa sababu yeye huugua saratani ya matiti hulazimika kwenda hospitali mara tatu kwa wiki ili kudungwa sindano mbali na kutibiwa kwa kutumia kemikali.
Anaongezea kwamba kwa muda mrefu hakuweza kusimama kwa miguu miwili na kuvaa suruali ndefu, ''nilikuwa nikitembea kwa kiti cha magurudumo''.
Anasema kwamba hakuweza kutembea na kwamba nywele alizo nazo sio nywele zake asilia.
Habari ya mwanamke huo imewagusa watu wengi ulimwenguni.
Anasema kwamba anatumia habari yake kuwapa moyo wanaougua kwamba maisha sio mabaya sana.
''Mbali na maisha na kifo mambo mengine yote ni madogo''.
Anasema kwamba watu wengi wanaougua huwa na wasiwasi wataishi kwa muda gani na lini watafariki ama iwapo matibabu wanayopata yanafanya kazi.
''Lakini mimi nawashauri kwamba usiwe na wasiwasi kwa sababu hujui, kwa hivyo kwa nini usijiliwaze''?
Source:BBCSwahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni