Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amewatahadharisha mashujaa wa vita vya uhuru ambao wameonya kuwa huenda wakakataa kuunga mkono serikali yake kufuatia mporomoko mkubwa zaidi wa uchumi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Mashujaa hao wanaonya kuwa watakataa kumuunga Mugabe mkono endapo hataweka mikakati ya kukomesha ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi uliokithiri mipaka na kusababisha maandamano makubwa zaidi.
Rais Mugabe aliwaonya mashujaa hao alipokuwa akihutubia umati wa wafuasi wa chama tawala cha Zanu-PF.
Aidha rais huyo aliwataka viongozi wa chama cha mashujaa kuwachagua viongozi wapya.
Mugabe alidai kuwa viongozi wa mashujaa hao wa vita vya ukombozi kutoka mikononi mwa wakoloni kuwa walikuwa wameshawishiwa na mataifa ya magharibi.
Shinikizo kwa rais huyo mwenye umri wa miaka 92 akabiliane na mfumuko wa bei ya vyakula na kudorora kwa uchumi wa taifa.
Rais Mugabe hata hivyo ameahidi kuwania awamu mpya ya utawala katika uchaguzi wa mwaka wa 2018.
Baadhi ya viongozi wa chama cha Zanu-PF wameanza kung'ang'ania madaraka.
Mugabe ameonya kuwa wale ambao wanaendeleza maandamano yaliyoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni huenda wakafungwa jela kwani taifa hilo halina haja ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Mashujaa hao ndio walioongoza uvamizi wa mashamba ya wazungu mwaka wa 2000.
SOURCE:BBCSwahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni