YoungConciousâ„¢

Be Updated on the World of Sports, latest News and Entertainment Stories.

Propellerads

Breaking News

Translate

Welcome to Young concious .blogspot.com ==>>Feel free to leave your comment

Jumanne, 27 Agosti 2013

MO DEWJI BILIONEA TISHIO

-AFUNIKA 10 BORA YA MABILIONEA VIJANA AFRIKA
Tanzania haipo nyuma tena. Mfanyabiashara mzalendo, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameitoa kimasomaso kwa kuongoza orodha ya mabilionea 10 vijana barani Afrika. Mtanzania mwingine, Patrick Ngowi, yumo hivyo kuzidi kuing’arisha ardhi yenye Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Ziwa Tanganyika na vivutio vingine lukuki.
1. MOHAMMED DEWJI, Tanzania
Kwa mujibu wa Jarida la Forbes Afrika, Dewji a.k.a Mo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini (CCM), anaongoza orodha ya vijana mabilionea Afrika kwa sababu kwa mwaka kampuni yake ya Mohammed Enterprises Ltd (METL) inayomiliki viwanda vingi nchini, inaingiza pato linalofikia dola milioni 85 (shilingi bilioni 136).
Forbes, limemnukuu Mo mwenyewe akisema kwamba mwaka 1999 kampuni yake ilikuwa imeshatengeneza faida ya dola milioni 30 (shilingi bilioni 48) lakini kwa sasa ikiwa ni zaidi ya miaka 12 baadaye, METL inatengeneza dola bilioni 1.1 (shilingi trilioni 1.8).
Mo, 38, ambaye ni mtoto wa bilionea mkubwa Tanzania, Gulam Dewji, ameliambia Forbes kuwa kati ya miaka mitano au 10 ijayo, anatarajia kutengeneza faida inayofikia dola bilioni 5 (shilingi trilioni 8). Kwa jumla, METL imeajiri wafanyakazi 24,000.
2. IGHO SANOMI, Nigeria
Umri wake ni miaka 38, utajiri wake umetokana na biashara ya mafuta ya ndege, petroli na kadhalika. Utajiri wake haujafafanuliwa sana, ila yapo maelezo kwamba makampuni yake, Taleveras Group, yanatengeneza wastani wa dola bilioni 1 (shilingi trilioni 1.6) kwa mwaka.
3. QUINTON VAN DER BURGH, Afrika Kusini
Anamiliki makampuni ambayo yapo chini ya mwavuli wenye jina la Quinton van der Burgh Investments. Biashara yake kubwa ni madini. Umri wake ni miaka 36 na utajiri wake unakadiriwa kufikia dola bilioni 1 (shilingi trilioni 1.6).
4. GERALD WAMALWA, Kenya
Chanzo cha utajiri wake ni uhandisi na ukandarasi. Mwaka 2003, akiwa na umri wa miaka 28, aliacha kazi aliyokuwa ameajiriwa kama mhandisi na kuanzisha kampuni yake inayoitwa Mellech. Leo hii, Mellech Engineering & Construction inatajwa kama moja ya makampuni makubwa ya uinjinia na ukandarasi Afrika Mashariki. Engineering & Construction. Pato lake kwa mwaka linakadiriwa kufikia dola milioni 45 (shilingi bilioni 72).
5. SIBONGILE SAMBO, Afrika Kusini
Huyu ni mwanamke wa shoka, mtaalamu wa vifaa vya anga. Mwaka 2004, akiwa na umri wa miaka 30, alianzisha kampuni inayohusika na matengenezo ya vifaa vya anga inayoitwa SRS Aviation. Kuanzia hapo ameweza kupiga hatua kubwa ambayo imemuwezesha kuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola milioni 219 (zaidi ya shilingi bilioni 350).
6. KHANYI DHLOMO, Afrika Kusini
Ni mwanamke mwenye heshima kubwa nchini Afrika Kusini. Akiwa na umri wa miaka 20, alianza kama mtangazaji katika Shirika la Habari Afrika Kusini (SABC), miaka miwili baadaye akateuliwa kuwa mhariri wa jarida maarufu la True Love ambalo alilipandisha kutoka usambazaji wa nakala 70,000 hadi 140,000.
Mwaka 2007, alianzisha kampuni ya habari inayoitwa Ndalo Media ambayo ilifanya kazi kwa ushirikiano na Jarida la Media 24 linalomilikiwa na Naspers ambayo ni kampuni kubwa ya habari Afrika. Ndalo Media lilichapisha Majarida ya Destiny na Destiny Man ambayo yamemuwezesha kuwa tajiri. Kwa sasa, Khanyi anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia dola milioni 190 (shilingi bilioni 304). Kwa sasa ana umri wa miaka 38.
7. KEN NJOROGE, Kenya
Utajiri wake umetokana na teknolojia ya simu za mkononi baada ya kuanzisha huduma inayoitwa Cellulant. Alianzisha mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 29. Kwa sasa Cellulant imeenea nchi nane za Afrika, Kenya, Tanzania, Ghana, Zambia, Nigeria, Malawi na Botswana. Mapato yake kwa mwaka yanakadiriwa kuwa dola milioni 120 (shilingi bilioni 192). Kwa sasa ana umri wa miaka 38.
8. COLLIN THORNTON, Afrika Kusini
Mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 20, alikatisha masomo Chuo Kikuu Witwatersrand, alipokuwa anasomea shahada ya Sayansi ya Kompyuta. Akaungaunga kwa marafiki na kupata dola 1000 (shilingi milioni 1.6) ambazo alizitumia kutangaza kampuni yake inayoitwa Dial-A-Nerd ambayo inajihusisha na utoaji wa huduma za kompyuta. Kwa sasa, kampuni hiyo inaingiza kwa mwaka dola milioni 10 (shilingi bilioni 16).
9. PATRICK NGOWI, Tanzania
Kijana mdogo wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28. Utajiri wake unatokana na biashara ya nishati mbadala inayotokana na mwanga wa jua. Ni mwanzilishi wa Kampuni ya Helvetic Solar, inayoongoza kwa utoaji wa nishati mbadala Afrika Mashariki. Mapato yake kwa mwaka yanakadiriwa kuwa dola milioni 7 (shilingi bilioni 11.2).
10. ALAN KNOTT-CRAIG JR., Afrika Kusini
Chanzo cha utajiri wake ni teknolojia na uwekezaji. Ana umri wa miaka 37, ndiye mwanzilishi wa Kampuni ya World Of Avatar (WOA).  Mwaka 2011, kampuni hiyo ilinunua huduma ya SMS katika simu za mkononi inayoitwa Mxit, vilevile ilijipatia dola milioni 50 (shilingi bilioni 80) kutoka Naspers kama malipo yake ya matangazo. Kwa sasa WOA ina wateja zaidi ya milioni 200.
Views: 250

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Propellerads