Duru kutoka
Senegal, zinasema kuwa watu wanane wameuwawa katika kisa cha
kukanyagana, baada ya vurumai kutokea wakati wa mchuano wa mechi ya
kandanda, kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Dakar.
Shirika rasmi la
habari la serikali ya nchi hiyo- (APS), linasema kwamba mashabiki wa
timu mbili za soka, walikabiliana baada ya mchuano wa soka uliochezewa
katika uwanja wa michezo wa Demba Diop stadium, kumalizika.Ukuta uliporomoka wakati ambapo idadi kubwa ya watu walipokuwa wakiondoka kwa kasi uwanjani.
Kisa hicho kilitokea wakati wa fainali ya kuwania kombe la ligi kuu nchini humo, kati ya timu ya soka ya Stade de Mbour na Union Sportive Ouakam.
Mapigano yalianza kati ya mashabiki wa timu hizo mbili hasimu, hatua iliyowachochea maafisa wa polisi kuwarushia vitoa machozi. Hatua hiyo ilisababisha taharuki kubwa miongoni mwa mashabiki ambao walianza kukimbia na kusababisha mkanyangano, na kuporomoka kwa ukuta.
Baadhi ya mashabiki walirusha kila aina ya vifaa yakiwemo mawe.
Picha zinazosambazwa mitandaoni, zinaonesha watu wakikurupuka na kujaribu kupanda juu ya ukuta mfupi, huku wakizungukwa na wingu kubwa wa moshi wa vitoa machozi.
Runinga ya taifa ya nchi hiyo, inasema kuwa, magari ya huduma za dharura na vikosi vya zima moto vilifika maeneo ya tukio hilo.
SOURCE:BBCSwahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni