Wanafunzi wa shule ya msingi ya Kenyatta Golf Course Academy jijini Nairobi, waliwashangaza wengi baada ya kuyaweka madawati barabarani mapema leo na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Wanafunzi hao, wakiwa kwenye sare zao rasmi za shule, waliimba na kujipanga kwa sehemu mbalimbali za barabara.
Walimu na wazazi wao nao walijiunga na wanafunzi wakiimba, "tunataka shule yetu, tunahitaji kutumia shule yetu''.
Shule hiyo inadaiwa kubomolewa wikendi kufuatia mzozo wa ardhi iliyotumika kujenga shule hiyo.
Wanafunzi hao wliondoka barabarani baadaye kwa hiari yao wakiwa na matumaini hali hiyo itasuluhishwa.
Zaidi ya shule elfu 24 za umma hazina hatimiliki ya ardhi zinazotumika na shule hizo na hilo limetajwa kutishia elimu ya watoto kwani shule 11,000 zimo hatarini kubomolewa au kunyakuliwa.
Maelfu ya watoto kutoka jamii maskini huenda wakakosa masomo kutokana na hali hiyo.
"Wamebomoa shule bila ilani, watoto wanataka kusoma, sijui tufanye nini, waliuliza''.
Walimu wa shule hiyo wameeleza wasiwasi wao kwani hatua hiyo imewaathiri kwa kuwaacha bila ajira.
Mnamo mwaka wa 2015, wanafunzi wa shule ya msingi ya Langata mjini Nairobi walifanya maandamano iliyopelekea kutupiwa mabomu ya kutoa machozi na mafisa wa polisi.
Wanafunzi hao walikuwa wakipinga kunyakuliwa kwa ardhi ya shule yao
SOURCE:BBCSwahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni