Kiongozi wa vijana
wa Chama cha Tanzania Girl Guides (TGGA), Dk. Helga Mutasingwa amefanya
kazi kubwa ya kuwashawishi Wananchi wa Mexico kuwa Mlima Kilimanjaro upo
Tanzania badala Kenya.
Dk. Mutasingwa ambaye alikuwa nchini
Mexico kwa mafunzo ya miezi minne ya kubadilishana uzoefu katika nyanja
za utamaduni na uongozi alitumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya
Tanzania.Akizungumza mara baada ya kuwasili jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, alisema kuwa moja ya mambo yaliyompa wakati mgumu ni kuwabadilisha wamexico kuwa Mlima Kilimanjaro upo Tanzania na si Kenya kama wanavyofahamu wao.
Alisema Wamexico wengi kwanza wanajua Afrika ni nchi, jambo ambalo pia ilibidi awaeleze kuwa siyo nchi bali ni bara kama yalivyo mabara mengine duniani na katika bara hilo kuna nchi nyingi na mojawapo ni Tanzania anayotokea yeye.
Alisema akiwa huko licha ya kuwafundisha kiswahili pia alitangaza vivutio vingi vya utalii vilivyopo nchini, ambapo aliwatajia wadudu, ndege wa kila aina na wanyama mbalimbali waliomo kwenye hifadhi za Serengeti, Ngorongoro Crater na nyinginezo.Pia aliwafundisha kuhusu utamaduni wa Tanzania zikiwemo ngoma za asili, upikaji wa vyakula vya kitanzania kama vile ndizi na pilau, mambo ambayo walifurahishwa nayo.
Dk. Mutasingwa alisema kuwa katika ziara hiyo ya mafunzo alikuwa na vijana wenzie wa Girl Guids kutoka Venezuela, Canada, Uingereza na Argentina na kwamba alipata wasaa wa kujifunza utamaduni wa mexico na kutoka nchi hizo zingine.Alisema kuwa alijifunza mambo mengi ikiwemo ujasiri wa kufanya kazi bila woga, siasa za mataifa mbalimbali, mambo ambayo ameahidi kuwafundisha vijana wenzie wa TGGA nchini Tanzania.
Source:BBCSwahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni