SERIKALI imesema Juni mwaka huu ni mwisho kwa askari wa usalama barabarani kutoza faini ya fedha kwa kuwatolea risiti za kieletroniki za papo hapo madereva wanaofanya makosa ya barabarani na badala yake, adhabu yake inahamia kwenye leseni.
Badala yake, madereva watakaokuwa wakifanya makosa barabarani watakuwa wanapunguziwa pointi kwenye leseni zao na makosa yanapozidi, madereva watanyang’anywa leseni zao.
Mpango huo ulitangazwa na Kikosi cha Usalama Barabarani miaka iliyopita, lakini ukachelewa kuanza. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni alibainisha hayo wakati akijibu hoja za wabunge wakati kupitishwa kwa bajeti ya Wizara hiyo juzi jioni.
“Juni mkataba wa kutoa pesa kwa makosa ya barabarani unamalizika, mkataba huo tuliingia na kampuni binafsi na kutokana na mfumo huo tukashindwa kuanzisha utaratibu wa kupunguza pointi, lakini tukishamaliza mkataba tutaanza utaratibu wa kuwapunguzia pointi madereva wanaofanya makosa barabarani,” alisema Naibu Waziri.
Kwa sasa, trafiki kote nchini wamekuwa wakitembea na mashine za kieletroniki za malipo (EFDs) na wamekuwa wakitoza faini za fedha kwa madereva wanaofanya makosa ya usalama barabarani papo hapo, badala ya zamani kuwaandikia taarifa ya malipo na kisha mkosaji anakwenda kulipa kituoni
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni